Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya Simba kinasema baada ya mechi ya juzi kocha mkuu wa Simba, Mbrazil Robertinho alithibitisha kuvutiwa na wachezaji wanne tu kati ya 11 waliocheza.
Wachezaji hao ni wale wasio na nafasi katika kikosi cha kwanza na kocha huyo alikaririwa na chanzo chetu akisema timu ilicheza vibaya na ilikosa nidhamu ya kujilinda ndiyo maana waliambulia matokeo mabaya yaliyowavua taji.
Kati ya mastaa wanne aliovutiwa na uwezo wao ni Kibu aliyeulizia umri wake na baada ya kuambiwa ni mchezaji aliye na umri chini ya miaka 30, alifurahi zaidi na kuweka wazi kuwa ni bonge la mchezaji aliyekosa kocha wa kumtengeneza.
Alisema Kibu ni mchezaji mzuri, anayetumia miguu yote na atahakikisha anauthibitishia umma kile alichokiona kikithibitishwa kupitia miguu yake.
Mchezaji mwingine aliyeuliziwa na Robertinho ni Jonas Mkude, aliyemsifia ni kiungo mzuri mkabaji anaweza kuisaidia timu ambayo amegundua imekosa nidhamu ya ukabaji na inacheza kwa kushambulia zaidi na kusahau kujilinda.
Kocha huyo pia alimtaja kijana aliyetoka timu ya vijana Michael Joseph, aliyesema ameona ana kitu na kwamba amekosa watu wa kumsaidia kuwa bora zaidi na alivyocheza.
Kocha huyo mwenye falsafa ya soka la kujilinda na kushambulia alimtaja pia Kennedy Juma, aliyecheza beki ya kati aliyesema ni aina ya wachezaji anaotamani kuwa nao ndani ya timu. “Kennedy anakaba kwenye nafasi ni mchezaji ambaye hatumii nguvu. Amefanya kazi nzuri uwanjani, ana umbo zuri na ni mrefu.